Rais mteule wa Marekani Donald Trump amesema biashara zake zitasimamiwa na kuendeshwa na wanawe wawili atakapokuwa rais.
Wanawe hao ni Donald junior na Eric, ambao tayari wamekuwa wakitekeleza majukumu muhimu katika uendeshaji wa baadhi ya biashara.Bw Trump amesema atawakabidhi biashara hizo kabla yake kuapishwa na kwamba hakuna mikataba mipya ya kibiashara ambayo itaingiwa na kampuni zake kipindi ambacho atakuwa anahudumu kama rais.
Wakosoaji wa rais huyo mteule wanasema bado atakuwa hatarini ya kutokea kwa mgongano wa maslahi iwapo hataachilia umiliki wa biashara zake.
Maafisa wa Trump wanaosimamia shughuli ya mpito wamesema kikao cha wanahabari ambacho kilitarajiwa wiki hii kuhusu nini itakuwa hatima ya kampuni zinazomilikiwa na Trump kimeahirishwa kwa muda usiojulikana kutoa muda wa kuandaliwa kwa mpango wa kina.
Msemaji wa Bw Trump amesema kikao hicho, ambacho kilitarajiwa kufanyika Alhamisi wiki hii, sasa kitafanyika Januari.
Donald Jr
Hayo yakijiri, Bw Trump amesema atamteua rais wa Goldman Sachs Gary Cohn kuwa mshauri wake mkuu wa masuala ya kiuchumi.Bw Cohn atakuwa mkuu wa Baraza la Uchumi wa Taifa White House, wadhifa ambao utamfanya kuwa mmoja wa watu wenye usemi zaidi kuhusu maamuzi ya kiuchumi katika ikulu ya White House.
Rais huyo wa Goldman ndiye mtu wa tatu kutoka kwenye benki hiyo kupewa wadhifa kwenye baraza la mawaziri la Bw Trump.
Steven Mnuchin, waziri mpya wa fedha, na Steve Bannon mshauri mkuu wa White House wote walikuwa maafisa watendaji katika benki ya Goldman.
Bw Trump pia amesema atatangaza uamuzi wake wa nani atakuwa waziri wa mambo ya nje katika serikali yake Jumanne asubuhi.
Maafisa wake wa mpito wamesema nafasi hiyo huenda ikapewa Rex Tillerson, afisa mkuu mtendaji wa Exxon Mobil.
CHANZO-BBC SWAHILI
No comments:
Post a Comment