Ads

test

Monday, January 16, 2017

Bulembo amfuata bintiye bungeni

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdallah Bulembo, ameteuliwa kuwa mbunge na Rais John Magufuli -uteuzi utakaomfanya aungane na mwanaye, Halima Bulembo, ndani ya mhimili huo wa dola.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu leo, Bulembo pamoja na Profesa Palamagamba Kabudi wameteuliwa na Rais Magufuli ambaye ametumia mamlaka yake ya kikatiba kufanya hivyo. Kwa mujibu wa Katiba, Rais anaruhusiwa kuteua wabunge 10 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Taarifa hiyo ya Ikulu ilieleza kwamba wabunge hao wapya wataapishwa kwa mujibu wa taratibu za Bunge la Tanzania linalotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu.
Kabudi ni mmoja wa wasomi maarufu hapa nchini na kwa muda mrefu alikuwa Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na pia alikuwa mmoja wa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.
Bulembo, zaidi ya wadhifa wake huo ndani ya CCM, alikuwa mmoja wa wasaidizi wa karibu wa Magufuli wakati akiwa mgombea urais wa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Katika miaka ya karibuni, Bunge la Tanzania halijawahi kuwa na mtu na mwanaye kwa wakati mmoja katika chombo hicho na Bulembo anakwenda kuweka historia ya aina yake na mwanaye huyo.

No comments:

Post a Comment